Jumapili, 18 Desemba 2016

MAANDALIZI YA KIDATO CHA KWANZA 2016

ILEJE YAJIANDAA KUPOKEA KIDATO CHA KWANZA 2017
Na;Daniel Mwambene, Songwe
Zikiwa zimebaki takribani wiki tatu ili kuanza mwaka mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini wilaya ya Ileje mkoani hapa imeanza kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi hao.

Katika kufanya hivyo,viongozi wa Halmshauri ya wilaya hiyo wamekuwa wakitembelea shule za sekondari zilizopo wilayani humo ili kujiridhisha,ambapo hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya aliongoza baadhi ya watendaji wake kutembelea shule zilizo na miradi ya SEDP.

Mkurugenzi huyo, Bw.Haji Mnasi aliweza kutembelea shule za sekondari Itale, Luswisi, Msomba na Bupigu zenye miradi ya ujenzi wa nyumba za walimu zitakazokuchukua familia sita (Six in One).

Pia kwenye baadhi ya shule hizo kuna miradi ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa vyoo vya kisasa.

Akizungumza na wakandarasi  katika shule alizotembelea mkurugenzi huyo aliwataka kumalizia kazi hiyo  mapema zaidi ili kuyafanya mazingira ya shule kuwa rafiki kwa walimu na wanafunzi yakienda sambamba na uwepo wa umeme unaosambazwa na serikali vijijini.

Naye mwandisi wa ujenzi wa wilaya hiyo, Bw.Hatibu Nunu aliwataka wakandarasi hao kufanya marekebisho katika maeneo aliyokuwa amebaini kukosewa kulingana na mikataba ya ujenzi waliyotiliana saini.
Sehemu ya uani ya nyumba ya walimu sekondari ya Itale(SEDP)
Mafundi wakiendelea na kazi kwenye jingo la madarasa sekondari ya Itale(SEDP)
Vyoo vinavyoengwa na SEDP sekondari ya Itale
Vyoo vilivyokuwepo kabla ya mradi wa SEDP

MGODI WA MAKAA YA MAWE KIWILA

VIONGOZI ILEJE WAKOMALIA MGODI WA KIWILA
Na Daniel Mwambene, Songwe
Katika kuhakikisha wilaya ya Ileje haiachwi nyuma katika masuala ya uwekezaji  viongozi wa  serikali wilayani humo wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili Mgodi wa Kiwila wa makaa ya mawe unaanze kazi.

Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara ili kuuhakikishia umma kuwa mgodi huo upo Ileje katika mkoa wa Songwe na si vinginevyo.

Juhudi hizo,zinalenga pia kuondoa fikra zilizokuwa zimejengeka kwa baadhi ya watu kuwa mgodi huo upo wilaya zingine kama vile ilivyo kwa baadhi ya watu kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya na kupelekea watalii kuingilia Kenya badala ya Tanzania.

Akiwa mgodini hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  hiyo Bw,Haj Mnasi alitaka kujihakikishia mawasiliano ya mara kwa yanakuwepo kati  ya wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe na si kupitia mkoa wa Mbeya kama ilivyokuwa imezoeleka.

Meneja Masoko na Utawala wa mgodi huo Bw.Boaz Gappi alimweleza mkurugenzi huyo kuwa,juhudi kubwa zinafanywa na STAMICO ili uzalishaji kwa kiasi uanze hapo mwakani.

Pia meneja huyo aliahidi kutoa ushirikiano  kwa viongozi wa wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe kuhakikisha kila kinachofanyika kinajulikana.

Hata hivyo alishauri kuwa na ushirikiano na wilaya ya Kyela ambako kuna nyumba za wafanyakazi na mgodi ukiwa Ileje zikitenganishwa na Mto Kiwila.

Katika bunge lililopita aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Mh,Aliko Kibona alikuwa akipiga kelele mara kwa mara kutaka mgodi huo kujulikana upo Ileje.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alipotembelea mgodi huo miezi kadhaa iliyopita aliwataka wadau wa mgodi huo walio nje ya mkoa wa Songwe kupitia mkoani Songwe na si mkoani Mbeya.

Wakazi wa Ileje wana matarajio makubwa juu ya vitu vinavyoweza kuitoa wilaya yao kiuchumi ukiwemo mgodi huo pamoja na uwepo wa barabara ya lami kutoka Momba hadi Isongole-Ileje na kuiunganisha Tanzania na Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haj Mnasi (kushoto) akisalimiana na Meneja wa mgodi huo Eng.Aswile Mapumba (kushoto).
Ramani ya mgodi wa Kiwila-Ileje mkoa wa Songwe
Meneja wa mgodi wa Kiwila Eng.Aswile Mapambo aliyeshika karatasi akitoa maelezo kwa viongozi wa wilaya ya Ileje
Moja ya majengo yaliyopo katika mgodi wa Kiwila
Karakana ya kuchongea vipuri mbalimbali vya mitambo
Jengo la utawala za mgodi wa Kiwila Ileje- Songwe

KILIMO CHA UMWAGILIAJI KATA YA BUPIGU

BUPIGU WATUMIA VEMA MTO MTUMBISI
Badala ya kusubiri mvua zinyeshe ndipo waingie mashambani,wakazi wa kijiji cha Bupigu wilayani Ileje mkoa wa Songwe wamejiingiza katika kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi hali inayowapunguzia makali ya maisha.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini juu ya uwepo wa mashamba madogo madogo ya mahindi, magimbi, mpunga, miwa, mbogamboga, ufugaji samaki na utunzaji wa mazingira.

Wakulima hao walieleza kuwa licha ya kunufaika na kilimo hicho kinachowapunguzia makali ya maisha  kumekuwa na tatizo la soko kwa mazao wanayozalisha hususani mbogamboga.
Kijana akiwa kwenye shamba la magimbi lililo kandokando ya Mto Mtumbisi.
Shamba la mahindi linalomwagiliwa Bupigu
Mama na watoto wake wakiandaa shamba la mpunga
Uoto wa asili aina ya makangaga uliotunzwa na kikundi cha Mkombozi
Mwanachama wa kikundi cha Mkombozi akiwa karibu na bwawa lao
Uoto wa asili wa kipekee katika kijiji hicho unaotunzwa vema usitoweke

Alhamisi, 1 Desemba 2016

ZOEZI LA UPIMAJI WA UWINGI WA MAJI KATIKA VISIMA LA PAMBA MOTO


Katika kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inakua na uhakika katika suala zima na upatikanaji wa kwa vijiji vyote ndani ya wilaya. Leo Idara ya Maji ikiongozwa na mkuu wa idara hiyo Eng. Marco Kalamu alisaidiana na wasaidizi wake akiwemo Eng. Briton walikuwa katika kijiji cha Mangwina kilichopo kata ya Bupigu.

Lengo la ziara yao lilikuwa ni kwenda kupima uwingi wa maji katika kisima hicho ili kujua uwezo wa kisima kabla ya kufunga pampu ya maji itakayokuwa inatumia solar.

Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika pia katika kijiji cha Mapogoro kilichopo katika katika kata ya Mbebe. Hii yote ni katika harakati za kupambana na tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya vijiji katika wilaya ya Ileje

Eng. Marko Kalamu Mkuu wa Idara ya Maji  akifuatilia kwa makini upimaji wa uwingi wa maji katika kisima cha maji cha kijiji cha Mangwina.