Jumapili, 18 Desemba 2016

MGODI WA MAKAA YA MAWE KIWILA

VIONGOZI ILEJE WAKOMALIA MGODI WA KIWILA
Na Daniel Mwambene, Songwe
Katika kuhakikisha wilaya ya Ileje haiachwi nyuma katika masuala ya uwekezaji  viongozi wa  serikali wilayani humo wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili Mgodi wa Kiwila wa makaa ya mawe unaanze kazi.

Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara ili kuuhakikishia umma kuwa mgodi huo upo Ileje katika mkoa wa Songwe na si vinginevyo.

Juhudi hizo,zinalenga pia kuondoa fikra zilizokuwa zimejengeka kwa baadhi ya watu kuwa mgodi huo upo wilaya zingine kama vile ilivyo kwa baadhi ya watu kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya na kupelekea watalii kuingilia Kenya badala ya Tanzania.

Akiwa mgodini hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  hiyo Bw,Haj Mnasi alitaka kujihakikishia mawasiliano ya mara kwa yanakuwepo kati  ya wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe na si kupitia mkoa wa Mbeya kama ilivyokuwa imezoeleka.

Meneja Masoko na Utawala wa mgodi huo Bw.Boaz Gappi alimweleza mkurugenzi huyo kuwa,juhudi kubwa zinafanywa na STAMICO ili uzalishaji kwa kiasi uanze hapo mwakani.

Pia meneja huyo aliahidi kutoa ushirikiano  kwa viongozi wa wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe kuhakikisha kila kinachofanyika kinajulikana.

Hata hivyo alishauri kuwa na ushirikiano na wilaya ya Kyela ambako kuna nyumba za wafanyakazi na mgodi ukiwa Ileje zikitenganishwa na Mto Kiwila.

Katika bunge lililopita aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Mh,Aliko Kibona alikuwa akipiga kelele mara kwa mara kutaka mgodi huo kujulikana upo Ileje.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alipotembelea mgodi huo miezi kadhaa iliyopita aliwataka wadau wa mgodi huo walio nje ya mkoa wa Songwe kupitia mkoani Songwe na si mkoani Mbeya.

Wakazi wa Ileje wana matarajio makubwa juu ya vitu vinavyoweza kuitoa wilaya yao kiuchumi ukiwemo mgodi huo pamoja na uwepo wa barabara ya lami kutoka Momba hadi Isongole-Ileje na kuiunganisha Tanzania na Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haj Mnasi (kushoto) akisalimiana na Meneja wa mgodi huo Eng.Aswile Mapumba (kushoto).
Ramani ya mgodi wa Kiwila-Ileje mkoa wa Songwe
Meneja wa mgodi wa Kiwila Eng.Aswile Mapambo aliyeshika karatasi akitoa maelezo kwa viongozi wa wilaya ya Ileje
Moja ya majengo yaliyopo katika mgodi wa Kiwila
Karakana ya kuchongea vipuri mbalimbali vya mitambo
Jengo la utawala za mgodi wa Kiwila Ileje- Songwe

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni