Jumatatu, 23 Januari 2017

Alhamisi, 12 Januari 2017

ILEJE WAADHIMISHA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KWA KUPANDA MITI

 Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh.Joseph Mkude akielekea eneo la upandaji miti

Na;Daniel Mwambene, Ileje
Watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wadau wengine wilayani Ileje wamesherekea Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupanda miti ili kuilinda wilaya hiyo dhidi ya ukame.

Zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh.Joseph Mkude pia lilihusisha watendaji wa ofisi yake, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wahudumu wa Ofisi pamoja na wadau wengine

Katika zoezi hilo Zaidi ya miti 200 iliyonunuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi ilipandwa katika eneo la boma jipya lililopo mjini Itumba ambayo ni makao makuu ya wilaya hiyo.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo kukamilika Mkuu wa Wilaya hiyo aliwataka watumishi kuwa na mwitikio chanya katika matukio kama hayo akisema kuwa yanaashiria uzalendo kwa Taifa.

‘’Ndugu zangu watumishi nawashukuru kuitikia wito wangu lakini naomba msichukulie matukio kama haya kuwa ni adhabu bali ni sehemu ya kazi inayotakiwa kukuongezea furaha katika moyo wako’’,alilisisitiza Mh. Mkude.

Alisema kuwa miti mingi iliyopo katika maeneo yanayotuzunguka haikufikia hapo bila juhudi za watu kufanyika kwa kuipanda au kuitunza,tabia ambazo alisema haina budi kuenziwe kwa kupanda miti kama zoezi lilivyofanyika.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Bw Haji Mnasi aliiahidi kusimama zoezi hilo na kuwataka viongozi wa halmashauri kufanya ukaguzi wa kila sehemu watakayotembelea ndani ya wilaya hiyo ili kujua utekeleji wa wa zoezu la upandaji miti unavyokwenda.

Mnasi aliongeza kuwa ni wajibu wa  kila kiongozi wa ngazi ya halmashauri hadi kitongoji kuhakikisha anafuatilia zoezi hilo kwa walio chini yake na mwananchi mmoja mmoja.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo Afande Fadhil Ishekazoba aliwataka wananchi kulinda miti iliyopandwa ili kuepukana na kufanya kazi ambayo haina matokeo chanya.

Alisema kuonesha kazi ilifanyika ni vema kuona ongezeko la miti inayokuwa katika maeneo mbalimbali  badala ya kuwa na idadi kubwa ya miti inayopandwa kila mwaka huku ikiishia kuliwa na mifugo pamoja na kuharibiwa na wanaokata kwaajili ya nishati ya kupikia.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi walioshiriki zoezi hilo Afisa Elimu Msingi Mwalimu Godwin Mkaruka aliahidi kuongeza idadi ya miti katika wilaya hiyo akitumia jeshi lake ambalo ni wanafunzi wakiongozwa na walimu wao

Alisema kuwa kila shule ilishaandaa kitalu cha miche tangu mwaka jana ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa huu wa Songwe Mh.Chiku Galawa aliyezitaka shule zote za msingi na sekondari kufanya hivyo.
 Katibu Tawala Wilaya ya Ileje Bi; Mary Joseph Marco akipanda mti
 Mmoja wa watumishi wa halmashauri akiwa kazini
 Mkuu wa Wilaya akipanda mti
 Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haji Mnasi akishiriki kupanda miti
 Watumishi wa serikali wakishiriki zoezi hilo


 Washiriki wa upandaji miti wakifurahia hotuba fupi ya Mkuu wa Wilaya
 Mkuu wa Polisi(OCD) wa Wilaya ya Ileje Afande Fadhil Majjid Ishekazoba akizungumza na walioshiriki upandaji wa miti akisisiza kuitunza




Jumatatu, 9 Januari 2017

MWANGALIE MKUU WA WILAYA YA ILEJE (Mh. JOSEPH MKUDE) AKIWA KWENYE MAJUKUMU YAKE


SERIKALI WILAYANI ILEJE YAHIMIZA UJENZI WA VYOO BORA

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakielekea kukagua choo cha wanafunzi shule ya sekondari Nakalulu

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh. Joseph Mkude amewagiza viongozi wa Serikali za Mitaa wilayani humo kuhakikisha wanasimamia vyema ujenzi wa vyoo bora katika shule na kuondokana na ujenzi wa vyoo vya muda.

Alitoa maagizo hayo wakati akiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama kukagua shughuli za ujenzi katika baadhi ya shule za sekondari ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza muhula wa kwanza wa masomo 2017.

Ziara hiyo ililenga katika kujiridhisha na maandalizi ya uwepo na ubora wa vyoo,vyumba vya madarasa na matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali.

Mh.Mkude akizungumza kwa nyakati tofauti katika shule za sekondari Itumba,Ileje,Nakalulu Kakoma na Mbebe alisikitishwa na hali aliyoiona katika baadhi ya shule hizo katika vyoo vya walimu na wanafunzi akisema kuwa haviendani na hadhi ya walimu.

Alisema kuwa vyoo vilivyopo katika shule za Nakalulu na Kakoma havichochei walimu kupenda mazingira ya kazi na haviendani na viwango vyao vya elimu ambayo ni mwanga kwa jamii inayozunguka shule.

‘’Vyoo vya shule vikiwa bora vinaweza kubadilisha ubora wa vyoo katika jamii kwa vile wanafunzi wakihitimu wataiga ujenzi huo na kuboresha zaidi na kabla ya mtu kuanza na ujenzi ya nyumba ya kuishi choo kiwe cha kwanza’’,alisema Mh. Mkude.

Akizungumza katika sekondari ya Mbebe aliwataka madiwani kuwatumia vema wataalam waliopo katika halmashauri hiyo kwenye masuala ya ujenzi na manunuzi ili kuijengea heshima halmashauri hiyo.

Kauli hiyo pia ilifuatia kasoro alizozibaini kwenye manunuzi ya mabati ya shule ya sekondari ya hiyo ambapo mabati 115 yalibainika kuwa chini ya viwango vinavyotakiwa katika majengo ya serikali hali iliyosababisha aagize yarudishwe kwa mwuzaji na kuchukua mabati yanayotakiwa.

Kwa upande wao, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo walipongeza juhudi zinazofanywa na kiongozi huyo,katika usimamizi wa shughuli za maendeleo kwa kufika maeneo husika bila kusubiri taarifa za mezani wakisema watendaji wengine hawana budi kuunga mkono juhudi hizo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, alimfananisha kiongozi huyo na baadhi ya viongozi waliotangulia ambao ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Stivin Kibona, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo marehemu Luhonzyo Siwale pamoja marehemu Mwangomo aliyekuwa Afisa Maliasili ambao alisema licha ya kuondoka hapa duniani bado matunda ya kazi zao yanaonekana.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mh.Gwalusako Kapesa alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jinsi anavyokuwa wazi hali aliyoielezea kuwa inaashiria ucha Mungu na ikifanywa na viongozi wengine itajenga hali kuaminiana katika kazi.

Pamoja na mambo mengine Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wote kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wanafanya hivyo na kufuatilia kwa kina wale wanaosena wamekwenda shule za binafsi badala ya zile za serikali.

Huku hali ikiwa mbaya kwa shule hizo kwa upnde wa vyoo bado kuna shule zimenufaika na ujenzi wa vyoo bora kwa ufadhili wa SEDP ambazo ni Luswisi,Itale,Msomba na Bupigu.
Vyoo vya walimu na wanafunzi katika sekondari ya Kakoma kilichojengwa chini ya viwango ambacho Mkuu wa Wilaya alikelezea kuwa kinadhalilisha watumishi wa Umma


 Mkuu wa Wilaya ya Ileje (kulia) akipata maelezo toka kwa Afisa Mtendaji wa kata ya Mbebe Nickson Mwashitete (kushoto) kuhusu matumizi ya fedha zilizotolewa na Halmashauri kwa shule ya sekondari Mbebe
 Mh.Mkude akiangalia ubora wa mabati kulingana na viwango vinavyotakiwa na serikali ambapo akisaidiwa na Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya alibaini mabati 115 yasiyokidhi viwango katika sekondari ya Mbebe.
 Wajumbe wa Kamati ya Ulinzina Usalama wakikagua jengo mojawapo katika sekondari ya Mbebe
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Mkuu Wilaya (hayupo pichani) ni ndani ya chumba cha darasa katika sekondari ya Mbebe.

Ijumaa, 6 Januari 2017

KAMATI YA ULINZI ILEJE KILA MMOJA KULEA MITI KUMI

 Mto Itumba ulivyofurika hadi kwenye mashamba ya wakazi wa kitongoji cha Kibanji katika kijiji cha Itumba

Na: Daniel Mwambene,Ileje
Katika kutimiza kwa vitendo zoezi la kila mwanafamilia kupanda miti kumi, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ileje mkoani Songwe kila mmoja amegawiwa miti kumi na kutakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuitunza.

Akigawa miche ya miti katika viwanja vya ofisi za wilaya Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Joseph Mkude aliwataka wajumbe hao kuhakikisha kila mmoja wao anapanda miche hiyo na kuilea ili iweze kukua na kufikia hatua nzuri.

“Tutakuwa tunakagua miti yenu kwanza kisha kwa Wakuu wa Idara wote, Wah. Madiwani na wananchi wengine ambapo kila mwanafamilia anatakiwa kupanda na kuilea naagiza kila kiongozi kwenye ngazi yake ahakikishe anasimamia zoezi hilo”alisisitiza Mh,Mkude.

Katika mgao huo miche ya miti ya mbao,na kivuli iligawiwa kwa wajumbe hao ikiwa imenunuliwa na ofisi yake huku viongozi wa taasisi,makanisa na misikiti wakitakiwa kufanya hivyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa miche hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo aliahidi kulinda miti hiyo sanjali na kusimamia watendaji walio chini yake.

Huku hayo yakijili wakazi wa vitongoji vya Chafwonya na Kibanji katika kijiji cha Itumba baadhi yao wameonja  madhara ya kutoacha mita 60 toka kwenye mto zilizopo kesheria baada ya Mto 

Itumba kufurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata za Ndola na wilaya ya Mbeya Vijijini ambako ni chanzo cha mto huo.

Uchunguzi wetu ulibaini mto huo kufurika hadi kwenye mashamba ambayo yamegharimu wakulima maelfu ya fedha za mbolea za chumvi chumvi.
 Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh.Joseph Mkude (kulia) akimgawia miche Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Haji Mnasi (kulia)
 Sehemu ya miche ya miti waliyokabidhiwa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ileje
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiwa na sehemu ya miche waliyokabidhiwa na mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh Joseph Mkude.

Jumanne, 3 Januari 2017

KATIBU TAWALA MKOA WA SONGWE ATOA SOMO KWA WATUMISHI WA UMMA MKOANI SONGWE

Na Daniel Mwambene Songwe                           
Watumishi wa umma mkoani Songwe  wametakiwa kutulia katika vituo vyao vya kazi ili kuwatumikia wananchi na kuwapunguzia gharama za kuendesha familia zao.

Wito huo ulitolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Mh. Elia Tandu wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa Idara na vitengo katika  Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya hiyo akiwa katika ziara ya kikazi.

Mh. Tandu alisema kuwa kutotulia katika vituo vya kazi siku za mwisho wa juma kwa baadhi ya watumishi hao kwa kisingizio cha kusafiri kwenda kuona familia zao kuna athari kubwa kwa serikali,wananchi na kwa maisha ya mtumishi mwenyewe.

Alisema kuwa limekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya watumishi wa umma kusafiri nje ya wilaya zao na mkoa siku za mwisho wa juma na sikukuu bila kufuata taratibu za kisheria hali inayosababisha usumbufu kwa waajiri wao pindi wanapowahitaji katika kipindi hiki cha serikali ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu “Hapa Kazi tu”.

Aliongeza kuwa huduma kwa wananchi zinategemea sana uwepo wao wa karibu hivyo kukosekana kwao kunawaongezea wananchi ugumu wa maisha.

Pia aliwaambia watumishi hao kuwa, kuwa mbali na familia zao kwa kisingizio cha mazingira magumu ya vituo vya kazi kunawaongezea gharama za maisha ambazo hazina msingi wowote kwakuwa wanakuwa na bajeti za familia mbili kwa wakati mmoja sawa na mwanaume mwenye mitala (wake wawili).

Alisema kuwa kupangiwa katika maeneo hayo hawana budi kujua kuwa wana jukumu la kuzibadilisha jamii wanazozikuta badala ya kuendelea kulalamikia ugumu wa mazingira huku wao wakitakiwa kuwasaidia wananchi kuwa chachu ya maendeleo.

Akifafanua zaidi alisema kuwa mkoa wilaya nyingi za mkoa wa Songwe zina changamoto zinazotautiana hivyo serikali iliwatuma kutumia taaluma zao kwa kusaidiana na wananchi kuzikabiri changamoto hizo.

Aliongeza kuwa kwa mtumishi yeyete kuwa na fikra za kuhama huwa kunamchelewesha kimaisha hali aliyoielezea kuwa haina budi kuachwa kwa kuwa wamejikuta hawahami huku wakiwa wametumia rasilimali nyingi katika kutafuta uhamisho huo.

Alisema kuwa kwa mtumishi yeyote ili kulinda utulivu wa akili yake hana budi kukifanya kituo chake cha kazi kuwa ni makazi yake ya kudumu hali itakayomwongezea ubunifu katika mambo anayoyafanya kila siku.

Akizungumza na watumishi wa kada mbalimbali katika wa halmashauri hiyo kwenye Ukumbi wa Mwala mjini Itumba Katibu Tawala huyo aliwataka watumishi hao kuzingatia maadli ya utumishi wa umma nakuepukana na vitendo vyote vinavyoweza kupunguza kasi ya utendaji wa serikali ya awamu hii yenye kupigania maslahi ya wanyonge.

Alisema kuwa mshikamano baina ya watumishi wa idara mbalimbali ni silaha itakayoupeleka mkoa wa Songwe mahali panapotakiwa na taifa letu lenye kuijenga Tanzania ya viwanda.
Aliwataka watumishi wa mkoa wa Songwe kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito ambapo serikali inashughulikia uhalali wa watumishi wa umma kwa kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya bandia (feki).

Kwa upande wao watumishi hao waliomba serikali iharakishe mazoezi ya uhakiki wa watumishi ili wale wanaotaka kuhama kwasababu za msingi waweze kufanya hivyo.
  
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Mh.Elia Tandu (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh. Joseph Mkude (kulia) alipowasili ofisi za wilaya hiyo

 Mh. Elia Tandu akizungumza na watumishi kwenye Ukumbi wa Mwala uliopo shule ya sekondari ya Itumba
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe kweny Ukumbi wa Mwala

VITUKO NDANI YA MTO SONGWE WILAYANI KYELA

Na;Daniel Mwambene Songwe
Waswahili husema kuwa” Macho hayana pazia”haya yalinikuta siku chache zilizopita nikielekea Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwila uliopo Ileje katika mkoa wa Songwe.

Macho yangu pekee hayakutosha kuweza kuona na kutunza kumbukumbu za kudumu juu ya mambo niliyoyaona katika safari ya kuelekea katika mgodi huo nililazimika kutumia kamera ili kila kitu kisiweze kupotea nikisafiri masaa kadha kutoka Itumbamakao makuu ya wilaya ya Ileje kwa kuzipita wilaya za Kyela na Rungwe na kurudi tena Itumba.

Mzunguko huo mrefu unawatesa Wanaileje wengi ambao hutaka kutembelea mgodi wao ama kwa kutalii ,mafunzo au kwa kazi maalum kwasababu tu ya miundombinu mibovu inayowalazimisha kupitia wilaya za Kyela na Rungwe, ambapo viongozi wa sasa wa wilaya hiyo wamesema inatosha wakichukua hatua za ujenzi wa barabara kupitia Ngulugulu na mkakati wa ujenzi wa daraja kule Landani.

Katika safari hiyo yapo mengi niliyoyaona na kupata maelezo juu ya uwepo wake nikiamini kwa pamoja tunaweza kuchukua hatua iwapo uwepo wake ni wa faida au  hasara.Tafadahali fuatilia mfululizo wa picha hizi na maelezo yake kwa ufupi.

Ni kwenye kilele cha Mlima Kaburo barabara ya Ndembo-Ileje kwenda Kyela 
Mmoja wa wavamizi wa msitu wa mlima Kaburo alinashwa na kamera yetu akiwa kwenye shughuli haramu ya uchomaji mkaa katika pori hilo



Uharibifu unaofanywa na wavamizi wanaochoma mkaa mlima Kaburo kunapunguza miti ya asili na kuharibu mandhari ya mlima huo 
Baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Walaya ya Ileje wakiwa ndani ya msitu wa  Kaburo kuangalia usalama wake


Uharibifu wa mazingira jinsi ulivyochangia kuharibu mandhari ya Mto Kiwila juhudi kubwa zinahitajika ili kurejesha hali yake 

 Lori aina ya Fuso (maarufu kama Mwalamusha) likipandisha Mlima Kaburo kutoka Kyela kwenda Ileje
Waweza kusema ni michezo ya kitoto katika maji kwa kutumia mashina ya migomba, hali haiko hivyo inasemekana njia hiyo ni ya kusafirisha mbao katika Mto Songwe wilayani Kyela mkoa wa Mbeya ambapo watu wazima huwatumia watoto kusafirisha mbao kwa kufungwa pamoja na mashina ya migomba kama kiini macho ili kukwepa ushuru pamoja na mkono wa serikali kwa ujumla 




 Upande wa Malawi unavyoonekana katika mpaka wa Kasumulu (border) wilayani Kyela
 Upande wa Malawi unavyoonekana katika mpaka wa Kasumulu (border) wilayani Kyela
 Biashara ya maembe Busale-Kyela ambapo ndo moja ilikuwa ikiuzwa Tzsh.1000

 Ramani ya mgodi wa Kiwila,mbele ni majengo ya utawala na kiwanda ,nyuma ni Mlima Kaburo ambao una zaidi ya tani milioni 30 za makaa ya mawe ambazo bado hazijachimbwa
 Moja ya viberenge au treni zilizokuwa zikibeba makaa ya mawe kikiwa kwenye njia yake(reli)
 Gari yaliyochakaa kwasababu ya kutelekezwa kutokana na kiwanda (mgodi) kusimama uzalishaji
 Mlango wa kuingia ndani ya mgodi wa Kiwila
 Moja ya mitambo iliyochakaa kutokana na kutofanya kazi kwa muda mrefu
 Sehemu ya uzalishaji umeme katika mgodi wa Kiwila
 Chumba cha kuongoza mitambo ya kuzalisha umeme mgodini hapo
 Ndani ya karakana ya mgodi ambapo ilikuwa ikizalisha vipuli (spea) mbalimbali za mitambo


 Jengo la utawa la katika mgodi wa Kiwila



 Moja ya majengo maarufu sana mgodini hapo.