Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakielekea kukagua choo cha wanafunzi shule ya
sekondari Nakalulu
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh. Joseph Mkude amewagiza viongozi
wa Serikali za Mitaa wilayani humo kuhakikisha wanasimamia vyema ujenzi wa vyoo
bora katika shule na kuondokana na ujenzi wa vyoo vya muda.
Alitoa maagizo hayo wakati akiongoza Kamati ya Ulinzi na
Usalama kukagua shughuli za ujenzi katika baadhi ya shule za sekondari ikiwa ni
siku moja kabla ya kuanza muhula wa kwanza wa masomo 2017.
Ziara hiyo ililenga katika kujiridhisha na maandalizi ya uwepo
na ubora wa vyoo,vyumba vya madarasa na matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa
na serikali.
Mh.Mkude akizungumza kwa nyakati tofauti katika shule za
sekondari Itumba,Ileje,Nakalulu Kakoma na Mbebe alisikitishwa na hali aliyoiona
katika baadhi ya shule hizo katika vyoo vya walimu na wanafunzi akisema kuwa
haviendani na hadhi ya walimu.
Alisema kuwa vyoo vilivyopo katika shule za Nakalulu na
Kakoma havichochei walimu kupenda mazingira ya kazi na haviendani na viwango
vyao vya elimu ambayo ni mwanga kwa jamii inayozunguka shule.
‘’Vyoo vya shule vikiwa bora vinaweza kubadilisha ubora wa
vyoo katika jamii kwa vile wanafunzi wakihitimu wataiga ujenzi huo na kuboresha
zaidi na kabla ya mtu kuanza na ujenzi ya nyumba ya kuishi choo kiwe cha kwanza’’,alisema
Mh. Mkude.
Akizungumza katika sekondari ya Mbebe aliwataka madiwani
kuwatumia vema wataalam waliopo katika halmashauri hiyo kwenye masuala ya
ujenzi na manunuzi ili kuijengea heshima halmashauri hiyo.
Kauli hiyo pia ilifuatia kasoro alizozibaini kwenye manunuzi
ya mabati ya shule ya sekondari ya hiyo ambapo mabati 115 yalibainika kuwa
chini ya viwango vinavyotakiwa katika majengo ya serikali hali iliyosababisha
aagize yarudishwe kwa mwuzaji na kuchukua mabati yanayotakiwa.
Kwa upande wao, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
walipongeza juhudi zinazofanywa na kiongozi huyo,katika usimamizi wa shughuli
za maendeleo kwa kufika maeneo husika bila kusubiri taarifa za mezani wakisema
watendaji wengine hawana budi kuunga mkono juhudi hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, alimfananisha kiongozi huyo
na baadhi ya viongozi waliotangulia ambao ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo
marehemu Stivin Kibona, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo marehemu Luhonzyo Siwale pamoja
marehemu Mwangomo aliyekuwa Afisa Maliasili ambao alisema licha ya kuondoka
hapa duniani bado matunda ya kazi zao yanaonekana.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Mh.Gwalusako Kapesa alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jinsi anavyokuwa wazi hali
aliyoielezea kuwa inaashiria ucha Mungu na ikifanywa na viongozi wengine
itajenga hali kuaminiana katika kazi.
Pamoja na mambo mengine Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi
wote kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza
kidato cha kwanza wanafanya hivyo na kufuatilia kwa kina wale wanaosena wamekwenda
shule za binafsi badala ya zile za serikali.
Huku hali ikiwa mbaya kwa shule hizo kwa upnde wa vyoo bado
kuna shule zimenufaika na ujenzi wa vyoo bora kwa ufadhili wa SEDP ambazo ni
Luswisi,Itale,Msomba na Bupigu.
Vyoo
vya walimu na wanafunzi katika sekondari ya Kakoma kilichojengwa chini ya
viwango ambacho Mkuu wa Wilaya alikelezea kuwa kinadhalilisha watumishi wa Umma
Mkuu wa Wilaya ya Ileje (kulia) akipata maelezo toka kwa Afisa Mtendaji wa kata ya Mbebe Nickson Mwashitete (kushoto) kuhusu matumizi ya fedha zilizotolewa na Halmashauri kwa shule ya sekondari Mbebe
Mh.Mkude akiangalia ubora wa mabati kulingana na viwango vinavyotakiwa na serikali ambapo akisaidiwa na Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya alibaini mabati 115 yasiyokidhi viwango katika sekondari ya Mbebe.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Mkuu Wilaya (hayupo pichani) ni ndani ya chumba cha darasa katika sekondari ya Mbebe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni