SALAMU
ZA MWAKA MPYA 2017 TOKA KWA MHESHIMIWA JOSEPH MODEST MKUDE (MKUU WA WILAYA YA
ILEJE)
Ndugu
Wananchi wote wa Wilaya ya Ileje tunapoelekea kumaliza Mwaka 2016 na kuukaribisha Mwaka
mpya 2017, napenda kutumia nafasi hii kutoa salamu za Mwaka mpya natoa pole
kwa maafa yaliyotokea katika Kata ya Mbebe.
Tarehe
21/12/2016 mnamo saa 9.02 alasiri kulitokea maafa hayo
yaliyosababishwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali katika Vijiji vya Mbebe,
Mapogoro na Shinji
Madhara
yaliyotokea ni pamoja na:-
·
Kifo cha mtoto wa miezi- 6
·
Kujeruhiwa kwa watu- 21
·
Kaya 162 kuezuliwa nyumba zao
·
Kuezuliwa kwa paa, madarasa mawaili shule ya
msingi Mbebe na athari zilizotokea kanisa la Moravian, T.A.G, Sabato, Last
church of god, Shinji United Church na Kanisa la Mizimu.
Kutokana
na hali hiyo natoa pole sana kwa Wananchi wote waliopatwa na maafa hayo na ninatoa wito kwa Ndugu, jamaa na marafiki na
wadau wengine wote kuendelea kuwasaidia waathirika ili warudi katika maisha yao
ya kawaida.
Aidha
katika kipindi hiki kumetokea misiba na matatizo mbalimbali katika Wilaya yetu kwa
mwaka huu 2016. Hivyo nawapa pole wote waliopatwa na matatizo mbalimbali.
Sambamba
na hilo napenda kusisitiza mambo yafuatayo kwa Wananchi wote wa Ileje.
1.
Ujenzi
wa nyumba bora
Katika ziara zangu Vijijini nimegundua kuwa nyumba
nyingi zinajengwa bila kufuata viwango vinavyotakiwa kama vile kuweka rinta,
kutumia miti au mbao ngumu na kutojenga misingi imara. Hivyo natoa wito kwenu
kujitahidi kujenga nyumba kwa kufuata viwango vinavyotakiwa.
2.
Kupanda
miti ili kuzuia upepo
Imebainika kuwa katika Wilaya yetu ya Ileje suala la
upandaji miti na utunzaji mazingira kiujumla bado halijapewa uzito unaostahili.
Miti inapandwa pale tu inapohitajika katika shughuli za kibiashara kama ilivyo
katika kata za Ngulilo, Lubanda na Ibaba.
Si hivyo tu bali suala la upandaji miti ni muhimu sana
katika utunzaji wa mazingira. Natoa wito kwenu wananchi katika msimu huu wa
mvua kuendelea kupanda miti ya kibiashara kama tulivyozoea ambapo nawataka kila
mtu kwenye kaya kupanda miti isiyopungua kumi (10) kwa kila mtu miti ikipandwa
kuzunguka makazi yetu itasaidia sana kukinga upepo usiharibu makazi yetu.
Kwa taasisi kama vile shule za msingi na sekondari, makanisa,
misikiti na sehemu nyingine za kazi hakikisheni mnapanda miti.
3.
Kilimo
Kufuatia utabiri wa hali ya hewa inayonyesha mvua
zitakuwa za wastani na chini ya wastani,hivyo kuashiria kuwa mvua zitakuwa
kidogo kwa uzalishaji.
Kwa mantiki hiyo, nasisitiza mnatakiwa kulima mazao
yanayostahimili ukame kama vile mihogo na viazi vitamu.
·
Kutumia vizuri mlicho nacho ili kuepuka
upungufu wa chakula kwene kaya zenu.
·
Kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo na
ushauri wa watalaam ili kuzalisha kwa tija.
·
Tumieni vema mabonde yenye unyevunyevu kwa
kuzalisha mazao mbalimbali.
4.
Usafi
wa mazingira
Napenda kuwakumbusha Wananchi juu ya umuhimu wa
kuendelea kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo yetu. Serikali imetuagiza
wote kushiriki kwenye usafi wa jumla kwa Nchi nzima siku ya kila jumamosi ya
mwisho wa Mwezi, Na kwa Mkoa wetu wa Songwe tumeagizwa kila jumamosi kwa kila
kaya kufanya usafi katika maeneo yake.
Nawashukuru wale wote wanajitokeza kufanya usafi katika
maeneo yenu. Hata hivyo bado wapo Wananchi wachache ambao hawajitokezi kufanya
usafi katika maeneo yao. Tayari nimetoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya kuwa ahakikishe suala la usafi linatekelezwa kwenye Kata
zote na kila mwisho wa Mwezi nipate taarifa ya utekelezaji wa usafi kwa Kata
zote.
Pia viongozi wote ngazi ya Wilaya,Tarafa, Kata, Vijiji
na Mitaa/Vitongoji wasimamie na kuhakikisha mitaa yao inakuwa safi. Usafi ni
muhimu sana hasa wakati huu wa msimu wa mvua ili kuepuka magonjwa ya kuhara na
pia kuondoa mazalio ya mbu.
5.
Hali
ya usalama
Ndugu wanachi tuendelee kudumisha amani na utulivu
katika Wilaya yetu. Hivyo ninatoa wito kwa yafuatayo ambayo yatakuwa ni
endelevu katika kuendelea kudumisha amani tuliyonayo.
i.
Kuendelea kuwa na mahusiano mazuri kati yetu
na Wilaya tunazopakana nazo. Ninatambua kwamba kuna baadhi ya maeneo ya mipaka
ya Wilaya yetu na Wilaya jirani kuna migogoro ya ardhi ambayo tunaendelea
kushughulikia na bila shaka yatapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
ii.
Kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na Nchi
jirani za Malawi na Zambia ambayo yapo kwa muda mrefu. Hivyo ninasisitiza
ushirikiano huu uendelee na kuwa wa kimanufaa sio wa kiuharifu.
iii.
Kuendelea kushirikiana miongoni mwa kaya na
kaya. Kwa kutoa taarifa mapema juu ya viashiria vya uvunjifu wa amani kwa raia.
iv.
Kuwa na ulinzi kati yetu wenyewe linapotokea
au kabla ya kutoka jambo baya kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama.
v.
Kujiepusha na vurugu zisizo na msingi kama
vile uchomaji tairi barabarani, upigaji wa fataki, ulevi wa kupindukia n.k
kwenye mkesha wa Mwaka mpya.
6.
Heri
ya Mwaka mpya 2017
Natumia
nafasi hii pia kuwatakia heri ya Mwaka mpya Wananchi wote wa Wilaya ya Ileje
ili mwenyezi Mungu atusaidie tumalize salama Mwaka 2016 na tuuone Mwaka mpya wa
2017. Nawatakia wote Mwaka 2017 uwe ni wenye Baraka na mafanikio kwenu. Tusherekee
kwa amani na utulivu sherehe za Mwaka mpya 2017.
Tunaposherekea
Mwaka mpya ni vizuri Wananchi tukumbuke kuwa bado tunayo majukumu mbele yetu ya
kuwaandaa na kuwapeleka watoto mashuleni hasa kwa wale wanaoenda kuanza kidato
cha kwanza, Darasa la kwanza na Wanafunzi wengine ili mahudhurio ya Shule yawe
mazuri kuanzia siku za mwanzo wa Mwaka. Maandalizi yafanyike mapema ili
wanafunzi waripoti shuleni kwa tarehe iliyopangwa.
NAWATAKIA
HERI YA MWAKA MPYA WA 2017.
MUNGU
IBARIKI ILEJE
MUNGU
IBARIKI SONGWE
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni