Na Daniel Mwambene
Songwe
Watumishi wa umma mkoani Songwe wametakiwa kutulia katika vituo vyao vya kazi
ili kuwatumikia wananchi na kuwapunguzia gharama za
kuendesha familia zao.
Wito huo ulitolewa na Katibu
Tawala wa Mkoa wa Songwe Mh. Elia Tandu wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa
Idara na vitengo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje
kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya hiyo akiwa katika ziara ya kikazi.
Mh. Tandu alisema kuwa kutotulia
katika vituo vya kazi siku za mwisho wa juma kwa baadhi ya watumishi hao kwa
kisingizio cha kusafiri kwenda kuona familia zao kuna athari kubwa kwa
serikali,wananchi na kwa maisha ya mtumishi mwenyewe.
Alisema kuwa limekuwa tatizo
kubwa kwa baadhi ya watumishi wa umma kusafiri nje ya wilaya zao na mkoa siku za
mwisho wa juma na sikukuu bila kufuata taratibu za kisheria hali inayosababisha
usumbufu kwa waajiri wao pindi wanapowahitaji katika kipindi hiki cha serikali
ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu “Hapa Kazi tu”.
Aliongeza kuwa huduma kwa
wananchi zinategemea sana uwepo wao wa karibu hivyo kukosekana kwao
kunawaongezea wananchi ugumu wa maisha.
Pia aliwaambia watumishi hao kuwa, kuwa mbali na familia zao kwa kisingizio cha mazingira magumu ya vituo vya kazi
kunawaongezea gharama za maisha ambazo hazina msingi wowote kwakuwa wanakuwa na
bajeti za familia mbili kwa wakati mmoja sawa na mwanaume mwenye mitala (wake
wawili).
Alisema kuwa kupangiwa katika
maeneo hayo hawana budi kujua kuwa wana jukumu la kuzibadilisha jamii
wanazozikuta badala ya kuendelea kulalamikia ugumu wa mazingira huku wao
wakitakiwa kuwasaidia wananchi kuwa chachu ya maendeleo.
Akifafanua zaidi alisema kuwa
mkoa wilaya nyingi za mkoa wa Songwe zina changamoto zinazotautiana hivyo
serikali iliwatuma kutumia taaluma zao kwa kusaidiana na wananchi kuzikabiri
changamoto hizo.
Aliongeza kuwa kwa mtumishi
yeyete kuwa na fikra za kuhama huwa kunamchelewesha kimaisha hali aliyoielezea
kuwa haina budi kuachwa kwa kuwa wamejikuta hawahami huku wakiwa wametumia
rasilimali nyingi katika kutafuta uhamisho huo.
Alisema kuwa kwa mtumishi yeyote
ili kulinda utulivu wa akili yake hana budi kukifanya kituo chake cha kazi kuwa
ni makazi yake ya kudumu hali itakayomwongezea ubunifu katika mambo
anayoyafanya kila siku.
Akizungumza na watumishi wa kada
mbalimbali katika wa halmashauri hiyo kwenye Ukumbi wa Mwala mjini Itumba
Katibu Tawala huyo aliwataka watumishi hao kuzingatia maadli ya utumishi wa
umma nakuepukana na vitendo vyote vinavyoweza kupunguza kasi ya utendaji wa
serikali ya awamu hii yenye kupigania maslahi ya wanyonge.
Alisema kuwa mshikamano baina ya
watumishi wa idara mbalimbali ni silaha itakayoupeleka mkoa wa Songwe mahali
panapotakiwa na taifa letu lenye kuijenga Tanzania ya viwanda.
Aliwataka watumishi wa mkoa wa
Songwe kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito ambapo serikali inashughulikia
uhalali wa watumishi wa umma kwa kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya
bandia (feki).
Kwa upande wao watumishi hao
waliomba serikali iharakishe mazoezi ya uhakiki wa watumishi ili wale wanaotaka
kuhama kwasababu za msingi waweze kufanya hivyo.
Mh. Elia Tandu akizungumza na watumishi kwenye Ukumbi wa Mwala uliopo shule ya sekondari ya Itumba
Watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe
kweny Ukumbi wa Mwala
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni