Jumapili, 18 Desemba 2016

MAANDALIZI YA KIDATO CHA KWANZA 2016

ILEJE YAJIANDAA KUPOKEA KIDATO CHA KWANZA 2017
Na;Daniel Mwambene, Songwe
Zikiwa zimebaki takribani wiki tatu ili kuanza mwaka mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini wilaya ya Ileje mkoani hapa imeanza kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi hao.

Katika kufanya hivyo,viongozi wa Halmshauri ya wilaya hiyo wamekuwa wakitembelea shule za sekondari zilizopo wilayani humo ili kujiridhisha,ambapo hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya aliongoza baadhi ya watendaji wake kutembelea shule zilizo na miradi ya SEDP.

Mkurugenzi huyo, Bw.Haji Mnasi aliweza kutembelea shule za sekondari Itale, Luswisi, Msomba na Bupigu zenye miradi ya ujenzi wa nyumba za walimu zitakazokuchukua familia sita (Six in One).

Pia kwenye baadhi ya shule hizo kuna miradi ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa vyoo vya kisasa.

Akizungumza na wakandarasi  katika shule alizotembelea mkurugenzi huyo aliwataka kumalizia kazi hiyo  mapema zaidi ili kuyafanya mazingira ya shule kuwa rafiki kwa walimu na wanafunzi yakienda sambamba na uwepo wa umeme unaosambazwa na serikali vijijini.

Naye mwandisi wa ujenzi wa wilaya hiyo, Bw.Hatibu Nunu aliwataka wakandarasi hao kufanya marekebisho katika maeneo aliyokuwa amebaini kukosewa kulingana na mikataba ya ujenzi waliyotiliana saini.
Sehemu ya uani ya nyumba ya walimu sekondari ya Itale(SEDP)
Mafundi wakiendelea na kazi kwenye jingo la madarasa sekondari ya Itale(SEDP)
Vyoo vinavyoengwa na SEDP sekondari ya Itale
Vyoo vilivyokuwepo kabla ya mradi wa SEDP

MGODI WA MAKAA YA MAWE KIWILA

VIONGOZI ILEJE WAKOMALIA MGODI WA KIWILA
Na Daniel Mwambene, Songwe
Katika kuhakikisha wilaya ya Ileje haiachwi nyuma katika masuala ya uwekezaji  viongozi wa  serikali wilayani humo wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili Mgodi wa Kiwila wa makaa ya mawe unaanze kazi.

Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara ili kuuhakikishia umma kuwa mgodi huo upo Ileje katika mkoa wa Songwe na si vinginevyo.

Juhudi hizo,zinalenga pia kuondoa fikra zilizokuwa zimejengeka kwa baadhi ya watu kuwa mgodi huo upo wilaya zingine kama vile ilivyo kwa baadhi ya watu kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya na kupelekea watalii kuingilia Kenya badala ya Tanzania.

Akiwa mgodini hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  hiyo Bw,Haj Mnasi alitaka kujihakikishia mawasiliano ya mara kwa yanakuwepo kati  ya wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe na si kupitia mkoa wa Mbeya kama ilivyokuwa imezoeleka.

Meneja Masoko na Utawala wa mgodi huo Bw.Boaz Gappi alimweleza mkurugenzi huyo kuwa,juhudi kubwa zinafanywa na STAMICO ili uzalishaji kwa kiasi uanze hapo mwakani.

Pia meneja huyo aliahidi kutoa ushirikiano  kwa viongozi wa wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe kuhakikisha kila kinachofanyika kinajulikana.

Hata hivyo alishauri kuwa na ushirikiano na wilaya ya Kyela ambako kuna nyumba za wafanyakazi na mgodi ukiwa Ileje zikitenganishwa na Mto Kiwila.

Katika bunge lililopita aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Mh,Aliko Kibona alikuwa akipiga kelele mara kwa mara kutaka mgodi huo kujulikana upo Ileje.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alipotembelea mgodi huo miezi kadhaa iliyopita aliwataka wadau wa mgodi huo walio nje ya mkoa wa Songwe kupitia mkoani Songwe na si mkoani Mbeya.

Wakazi wa Ileje wana matarajio makubwa juu ya vitu vinavyoweza kuitoa wilaya yao kiuchumi ukiwemo mgodi huo pamoja na uwepo wa barabara ya lami kutoka Momba hadi Isongole-Ileje na kuiunganisha Tanzania na Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haj Mnasi (kushoto) akisalimiana na Meneja wa mgodi huo Eng.Aswile Mapumba (kushoto).
Ramani ya mgodi wa Kiwila-Ileje mkoa wa Songwe
Meneja wa mgodi wa Kiwila Eng.Aswile Mapambo aliyeshika karatasi akitoa maelezo kwa viongozi wa wilaya ya Ileje
Moja ya majengo yaliyopo katika mgodi wa Kiwila
Karakana ya kuchongea vipuri mbalimbali vya mitambo
Jengo la utawala za mgodi wa Kiwila Ileje- Songwe

KILIMO CHA UMWAGILIAJI KATA YA BUPIGU

BUPIGU WATUMIA VEMA MTO MTUMBISI
Badala ya kusubiri mvua zinyeshe ndipo waingie mashambani,wakazi wa kijiji cha Bupigu wilayani Ileje mkoa wa Songwe wamejiingiza katika kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi hali inayowapunguzia makali ya maisha.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini juu ya uwepo wa mashamba madogo madogo ya mahindi, magimbi, mpunga, miwa, mbogamboga, ufugaji samaki na utunzaji wa mazingira.

Wakulima hao walieleza kuwa licha ya kunufaika na kilimo hicho kinachowapunguzia makali ya maisha  kumekuwa na tatizo la soko kwa mazao wanayozalisha hususani mbogamboga.
Kijana akiwa kwenye shamba la magimbi lililo kandokando ya Mto Mtumbisi.
Shamba la mahindi linalomwagiliwa Bupigu
Mama na watoto wake wakiandaa shamba la mpunga
Uoto wa asili aina ya makangaga uliotunzwa na kikundi cha Mkombozi
Mwanachama wa kikundi cha Mkombozi akiwa karibu na bwawa lao
Uoto wa asili wa kipekee katika kijiji hicho unaotunzwa vema usitoweke

Alhamisi, 1 Desemba 2016

ZOEZI LA UPIMAJI WA UWINGI WA MAJI KATIKA VISIMA LA PAMBA MOTO


Katika kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inakua na uhakika katika suala zima na upatikanaji wa kwa vijiji vyote ndani ya wilaya. Leo Idara ya Maji ikiongozwa na mkuu wa idara hiyo Eng. Marco Kalamu alisaidiana na wasaidizi wake akiwemo Eng. Briton walikuwa katika kijiji cha Mangwina kilichopo kata ya Bupigu.

Lengo la ziara yao lilikuwa ni kwenda kupima uwingi wa maji katika kisima hicho ili kujua uwezo wa kisima kabla ya kufunga pampu ya maji itakayokuwa inatumia solar.

Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika pia katika kijiji cha Mapogoro kilichopo katika katika kata ya Mbebe. Hii yote ni katika harakati za kupambana na tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya vijiji katika wilaya ya Ileje

Eng. Marko Kalamu Mkuu wa Idara ya Maji  akifuatilia kwa makini upimaji wa uwingi wa maji katika kisima cha maji cha kijiji cha Mangwina.

Jumatano, 30 Novemba 2016

WILAYA YA ILEJE YATAKIWA KUJIPANGA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI DHIDI YA VVU NA UKIMWI


Katibu Tawala  wa Wilaya ya Ileje akifungua kikao cha kupanga mikakati ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.

WILAYA YA ILEJE YATAKIWA KUJIPANGA DHIDI YA VVU NA UKIMWI
Na;Daniel Mwambene: Songwe

Katika  kupunguza maambukizi  mapya ya VVU na UKIMWI makundi mbalimbali wilayani Ileje yametakiwa kuchukua hatua za dhati katika kulikabiri janga hili ambalo lilishatangazwa na Awamu ya Tatu.

Hayo yalisemwa na wawakilishi wa makundi mbalimbali waliokuwa wakichangia kwenye kikao cha kupanga mikakati ya kupunguza maambukizi mapya katika wilaya hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri .

Mratibu wa TACAIDS mikoa ya Songwe na Mbeya Emamanuel Petro akisoma taarifa ya UKIMWI kitaifa na kimkoa aliwataka wajumbe hao kuwa na mkakati itakayokwenda sambamba na mikakati ya kimkoa  na kitaifa.

Henry Kayuni Mwenyekiti wa  Muungano wa Vikundi vya WAVIU wilayani Ileje aliwataka wananchi wote kujiepusha na unyanyapaa kwa wenye VVU na kuwataka watu wenye maambukizi hayo kujitangaza ili kuiokoa jamii badala ya kujificha wakiendelea kuambukiza.

Naye mwakilishi wa makundi ya dini katika mafunzo hayo Shekh wa wilaya hiyo Khamiss Simbeye aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kushikilia mafunzo ya dini zao.

Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI ya Halmashauri ya Wilaya hiyo Mh.Diwani Gwalusako Kapesa aliwataka wanafunzi ambao wapo majumbani baada ya shule kufunga wasitumie muda huo kujihusisha na vitendo vya ngono kwa kutumia mwanya kuwa mbali na sheria za shule.

Akifunga mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Najum Tekka aliwataka walimu wa shule za msingi na sekondari kuunda klabu za mapambano dhidi ya UKIMWI.


Tangu serikali ianzishe Sera ya UKIMWI ya mwaka 2001 maambukizi yamekuwa  yakipungua kutokana na mikakati inayotoa elimu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa

Mratibu wa TACAIDS mikoa ya Songwe na Mbeya Emmanuel Petro akiwezesha katika kikao hicho.

Kaimu Mkurugenzi Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Ileje Bi; Nujum Tekka akifunga kikao hicho.

Jumanne, 29 Novemba 2016

MATOKEO YA MTIHANI WA TAIFA DARASA LA SABA 2016 YATANGAZWA RASMI


MKOA WA SONGWE KUVALIA NJUGA  SEKTA YA ELIMU
Na;Daniel Mwambene, Songwe
Wakati ya kitangazwa matokeo jumla ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania, viongozi wa wilaya za mkoa wa Songwe wameahidi kufanya vema katika mwaka ujao ili kuondokana na aibu ya kuwa miongoni mwa mikoa 10 ya mwisho.

Ahadi hizo zilitolewa katika ukumbi wa sekondari ya Vwawa wakati Kamati ya Mkoa ya Uendeshaji wa Mitihani  ilipokuwa ikitoa matokeo jumla  kwa viongozi wa Halmashauri zote tano za mkoa huo.
Akisoma matokeo hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Eliya Ntandu aliwambia viongozi wa wilaya hizo kuwa mkoa wao umekuwa miongoni mwa mikoa 10 ambayo haikufanya vizuri.

Aliongeza kuwa hali hiyo imechangiwa na kufanya vibaya kwa kila wilaya ambako pia kulichangiwa na ufaulu duni wa shule moja moja ambao unagusa wadau mbalimbali wa elimu.

Katika matokeo hayo Halmashauri  ya Mji wa Tunduma imekuwa kinara, ikifuatiwa na Mbozi, huku nafasi  ya  tatu  ikikaliwa na Ileje, ya  nne  Songwe na mkiani ipo wilaya ya Momba.
Shule ya binafsi ya Ilasi imeonekana kufanya vizuri baada ya kutoa mwanafunzi wa kwanza kimkoa huku shule ya msingi Kambarage ya Hamashauri ya Wilaya ya Songwe ikiwa haina mwanafunzi hata mmoja atakayekwenda sekondari.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mh. Ubatizo Songa alitoa wito kwa Wanasongwe kutofurahia hali hiyo  na kuahidi kujipanga upya ili kuachana na kuondokana hiyo.
Aliongeza kuwa,upya wa mkoa kisiwe kisingizio cha kufanya mambo vibaya yanayoleta matokeo duni na kuuabisha mkoa.

Kauli hiyo, iliungwa mkono na Mwenyekiti  Kamati ya Uendeshaji Mitihani alipokuwa akifunga kika hicho alipowataka viongozi kwenda sehemu kwenye vituo vyao vya kazi ili kubaini mapungufu yaliyojitokeza kna kuyatautia ufumbuzi kulingana na mazingira ya kila halmashauri.


Mkoa wa Songwe ulianzishwa mwanzoni mwa mwaka huu ukiwa umemegwa toka mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa mipya ya Tanzania iliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni hapa nchini,mikoa mingine ni  Njombe,Simiyu,Geita na Katavi.

Viongozi wa mkoa wa wa Songwe wakijiandaa  kutoa matokeo  jumla ya mkoa ya Kumaliza Elimu ya Msingi 2016.

.Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe  akitoa maagizo wakati wa kufunga kikao hicho

Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Songwe akizungumza na wajumbe wa kikao hicho.

Mh. Mkuu wa Wilaya ya Ileje akichangia

Mh. Mwenyeki wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje akiongea

Wajumbe toka Halmashauri ya wilaya ya Mbozi

Wajumbe toka Halmashauri ya Wilaya ya Momba

HOSPITALI YA WILAYA YA ILEJE YAPATA MSAADA WA MASHUKA


HOSPITALI YA WILAYA YA ILEJE YAPATA MSAADA WA MASHUKA
Na;Daniel Mwambene,Songwe
Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa vifaa mbalimbali,hospitali ya Itumba imepokea mashuka 200 kutoka kwa mbunge wa  Jimbo la Uchaguzi la Ileje ikiwa ni sehemu ya mashuka 600  yatakayotolewa na mbunge huyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashuka hayo, Katibu wa  mbunge Deo Mulungu alisema kuwa mashuka mengine 400  yatakabidhiwa mara yatakapofikishwa jimboni humo siku chache zijazo ,hivyo kukamilisha jumla ya mashuka 600.

Katibu huyo alieleza kuwa,mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na juhudi za Mh.mbunge katika kutafuta wadau mbalimbali walio tayari kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Haji  Mnasi alipongeza juhudi hizo na kuahidi kusimamia matumizi sahihi ya mashuka hayo na kuwapunguzia kero wagonjwa amboa huhitaji faraja muda wote wawapo hospitalini.

Kaimu Mganga Mkuu wa  Wilaya hiyo Rowland Mroso akishukuru kwa niaba ya watumishi wa hospitali hiyo aliahidi kutunza mashuka hayo kwa mujibu wa taratibu za afya na aliomba kutochoka kutoa misaada pale mbunge huyo atakapoombwa tena.

Hata hivyo,bado hospitali hiyo inakabiliwa na matatizo lukuki ikiwemo kukosa mtaalam wa  kutumia mashine ya x-ray ambayo ilishanunuliwa.


Tangu kupewa kibali cha kuwa hospitali ya wilaya  wananchi wa tarafa ya Bulambya wamepunguziwa kero ya muda mrefu ambapo hapo awali walilazimika kusafiri hadi hospitali ya Isoko zaidi ya kilometa 60 au kwenda nchi jirani ya Malawi. 

Kaimu Mganga Mkuu akimshurukuru Katibu wa Mh.Mbunge

Maboksi yenye mashuka 200 kwa ajili ya hospitali ya Itumba ambayo ni hospitali ya wilaya Ileje

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Haji Mnasi (kushoto) akiwa  na Katibu wa Mh.mbunge(kulia) wakiwa katika eneo la hospitali kabla ya makabidhiano ya mashuka yaliyotolewa na Mh.Janet Mbene(mb).

Kaimu Mganga Mkuu Rowland Mroso (mwenye miwani) akishukuru kwa niaba ya watumishi wa hospitali hiyo na kuahidi kuyatunza vema.

Mkurugenzi akishukuru baada ya kupokea msaada huo akiahidi kusimamamia matumizi yake

Mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo Oscar Kaponda akishukuru kwa msaada huo na kuomba mbunge aendelee kutafuta wadau wanaoweza kusaidia vifaa vingine vinavyopungua ikwemo ‘’utra sound’