Jumatatu, 23 Januari 2017

Alhamisi, 12 Januari 2017

ILEJE WAADHIMISHA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KWA KUPANDA MITI

 Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh.Joseph Mkude akielekea eneo la upandaji miti

Na;Daniel Mwambene, Ileje
Watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wadau wengine wilayani Ileje wamesherekea Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupanda miti ili kuilinda wilaya hiyo dhidi ya ukame.

Zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh.Joseph Mkude pia lilihusisha watendaji wa ofisi yake, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wahudumu wa Ofisi pamoja na wadau wengine

Katika zoezi hilo Zaidi ya miti 200 iliyonunuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi ilipandwa katika eneo la boma jipya lililopo mjini Itumba ambayo ni makao makuu ya wilaya hiyo.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo kukamilika Mkuu wa Wilaya hiyo aliwataka watumishi kuwa na mwitikio chanya katika matukio kama hayo akisema kuwa yanaashiria uzalendo kwa Taifa.

‘’Ndugu zangu watumishi nawashukuru kuitikia wito wangu lakini naomba msichukulie matukio kama haya kuwa ni adhabu bali ni sehemu ya kazi inayotakiwa kukuongezea furaha katika moyo wako’’,alilisisitiza Mh. Mkude.

Alisema kuwa miti mingi iliyopo katika maeneo yanayotuzunguka haikufikia hapo bila juhudi za watu kufanyika kwa kuipanda au kuitunza,tabia ambazo alisema haina budi kuenziwe kwa kupanda miti kama zoezi lilivyofanyika.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Bw Haji Mnasi aliiahidi kusimama zoezi hilo na kuwataka viongozi wa halmashauri kufanya ukaguzi wa kila sehemu watakayotembelea ndani ya wilaya hiyo ili kujua utekeleji wa wa zoezu la upandaji miti unavyokwenda.

Mnasi aliongeza kuwa ni wajibu wa  kila kiongozi wa ngazi ya halmashauri hadi kitongoji kuhakikisha anafuatilia zoezi hilo kwa walio chini yake na mwananchi mmoja mmoja.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo Afande Fadhil Ishekazoba aliwataka wananchi kulinda miti iliyopandwa ili kuepukana na kufanya kazi ambayo haina matokeo chanya.

Alisema kuonesha kazi ilifanyika ni vema kuona ongezeko la miti inayokuwa katika maeneo mbalimbali  badala ya kuwa na idadi kubwa ya miti inayopandwa kila mwaka huku ikiishia kuliwa na mifugo pamoja na kuharibiwa na wanaokata kwaajili ya nishati ya kupikia.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi walioshiriki zoezi hilo Afisa Elimu Msingi Mwalimu Godwin Mkaruka aliahidi kuongeza idadi ya miti katika wilaya hiyo akitumia jeshi lake ambalo ni wanafunzi wakiongozwa na walimu wao

Alisema kuwa kila shule ilishaandaa kitalu cha miche tangu mwaka jana ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa huu wa Songwe Mh.Chiku Galawa aliyezitaka shule zote za msingi na sekondari kufanya hivyo.
 Katibu Tawala Wilaya ya Ileje Bi; Mary Joseph Marco akipanda mti
 Mmoja wa watumishi wa halmashauri akiwa kazini
 Mkuu wa Wilaya akipanda mti
 Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haji Mnasi akishiriki kupanda miti
 Watumishi wa serikali wakishiriki zoezi hilo


 Washiriki wa upandaji miti wakifurahia hotuba fupi ya Mkuu wa Wilaya
 Mkuu wa Polisi(OCD) wa Wilaya ya Ileje Afande Fadhil Majjid Ishekazoba akizungumza na walioshiriki upandaji wa miti akisisiza kuitunza




Jumatatu, 9 Januari 2017

MWANGALIE MKUU WA WILAYA YA ILEJE (Mh. JOSEPH MKUDE) AKIWA KWENYE MAJUKUMU YAKE


SERIKALI WILAYANI ILEJE YAHIMIZA UJENZI WA VYOO BORA

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakielekea kukagua choo cha wanafunzi shule ya sekondari Nakalulu

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh. Joseph Mkude amewagiza viongozi wa Serikali za Mitaa wilayani humo kuhakikisha wanasimamia vyema ujenzi wa vyoo bora katika shule na kuondokana na ujenzi wa vyoo vya muda.

Alitoa maagizo hayo wakati akiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama kukagua shughuli za ujenzi katika baadhi ya shule za sekondari ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza muhula wa kwanza wa masomo 2017.

Ziara hiyo ililenga katika kujiridhisha na maandalizi ya uwepo na ubora wa vyoo,vyumba vya madarasa na matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali.

Mh.Mkude akizungumza kwa nyakati tofauti katika shule za sekondari Itumba,Ileje,Nakalulu Kakoma na Mbebe alisikitishwa na hali aliyoiona katika baadhi ya shule hizo katika vyoo vya walimu na wanafunzi akisema kuwa haviendani na hadhi ya walimu.

Alisema kuwa vyoo vilivyopo katika shule za Nakalulu na Kakoma havichochei walimu kupenda mazingira ya kazi na haviendani na viwango vyao vya elimu ambayo ni mwanga kwa jamii inayozunguka shule.

‘’Vyoo vya shule vikiwa bora vinaweza kubadilisha ubora wa vyoo katika jamii kwa vile wanafunzi wakihitimu wataiga ujenzi huo na kuboresha zaidi na kabla ya mtu kuanza na ujenzi ya nyumba ya kuishi choo kiwe cha kwanza’’,alisema Mh. Mkude.

Akizungumza katika sekondari ya Mbebe aliwataka madiwani kuwatumia vema wataalam waliopo katika halmashauri hiyo kwenye masuala ya ujenzi na manunuzi ili kuijengea heshima halmashauri hiyo.

Kauli hiyo pia ilifuatia kasoro alizozibaini kwenye manunuzi ya mabati ya shule ya sekondari ya hiyo ambapo mabati 115 yalibainika kuwa chini ya viwango vinavyotakiwa katika majengo ya serikali hali iliyosababisha aagize yarudishwe kwa mwuzaji na kuchukua mabati yanayotakiwa.

Kwa upande wao, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo walipongeza juhudi zinazofanywa na kiongozi huyo,katika usimamizi wa shughuli za maendeleo kwa kufika maeneo husika bila kusubiri taarifa za mezani wakisema watendaji wengine hawana budi kuunga mkono juhudi hizo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, alimfananisha kiongozi huyo na baadhi ya viongozi waliotangulia ambao ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Stivin Kibona, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo marehemu Luhonzyo Siwale pamoja marehemu Mwangomo aliyekuwa Afisa Maliasili ambao alisema licha ya kuondoka hapa duniani bado matunda ya kazi zao yanaonekana.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mh.Gwalusako Kapesa alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jinsi anavyokuwa wazi hali aliyoielezea kuwa inaashiria ucha Mungu na ikifanywa na viongozi wengine itajenga hali kuaminiana katika kazi.

Pamoja na mambo mengine Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wote kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wanafanya hivyo na kufuatilia kwa kina wale wanaosena wamekwenda shule za binafsi badala ya zile za serikali.

Huku hali ikiwa mbaya kwa shule hizo kwa upnde wa vyoo bado kuna shule zimenufaika na ujenzi wa vyoo bora kwa ufadhili wa SEDP ambazo ni Luswisi,Itale,Msomba na Bupigu.
Vyoo vya walimu na wanafunzi katika sekondari ya Kakoma kilichojengwa chini ya viwango ambacho Mkuu wa Wilaya alikelezea kuwa kinadhalilisha watumishi wa Umma


 Mkuu wa Wilaya ya Ileje (kulia) akipata maelezo toka kwa Afisa Mtendaji wa kata ya Mbebe Nickson Mwashitete (kushoto) kuhusu matumizi ya fedha zilizotolewa na Halmashauri kwa shule ya sekondari Mbebe
 Mh.Mkude akiangalia ubora wa mabati kulingana na viwango vinavyotakiwa na serikali ambapo akisaidiwa na Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya alibaini mabati 115 yasiyokidhi viwango katika sekondari ya Mbebe.
 Wajumbe wa Kamati ya Ulinzina Usalama wakikagua jengo mojawapo katika sekondari ya Mbebe
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Mkuu Wilaya (hayupo pichani) ni ndani ya chumba cha darasa katika sekondari ya Mbebe.

Ijumaa, 6 Januari 2017

KAMATI YA ULINZI ILEJE KILA MMOJA KULEA MITI KUMI

 Mto Itumba ulivyofurika hadi kwenye mashamba ya wakazi wa kitongoji cha Kibanji katika kijiji cha Itumba

Na: Daniel Mwambene,Ileje
Katika kutimiza kwa vitendo zoezi la kila mwanafamilia kupanda miti kumi, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ileje mkoani Songwe kila mmoja amegawiwa miti kumi na kutakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuitunza.

Akigawa miche ya miti katika viwanja vya ofisi za wilaya Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Joseph Mkude aliwataka wajumbe hao kuhakikisha kila mmoja wao anapanda miche hiyo na kuilea ili iweze kukua na kufikia hatua nzuri.

“Tutakuwa tunakagua miti yenu kwanza kisha kwa Wakuu wa Idara wote, Wah. Madiwani na wananchi wengine ambapo kila mwanafamilia anatakiwa kupanda na kuilea naagiza kila kiongozi kwenye ngazi yake ahakikishe anasimamia zoezi hilo”alisisitiza Mh,Mkude.

Katika mgao huo miche ya miti ya mbao,na kivuli iligawiwa kwa wajumbe hao ikiwa imenunuliwa na ofisi yake huku viongozi wa taasisi,makanisa na misikiti wakitakiwa kufanya hivyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa miche hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo aliahidi kulinda miti hiyo sanjali na kusimamia watendaji walio chini yake.

Huku hayo yakijili wakazi wa vitongoji vya Chafwonya na Kibanji katika kijiji cha Itumba baadhi yao wameonja  madhara ya kutoacha mita 60 toka kwenye mto zilizopo kesheria baada ya Mto 

Itumba kufurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata za Ndola na wilaya ya Mbeya Vijijini ambako ni chanzo cha mto huo.

Uchunguzi wetu ulibaini mto huo kufurika hadi kwenye mashamba ambayo yamegharimu wakulima maelfu ya fedha za mbolea za chumvi chumvi.
 Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mh.Joseph Mkude (kulia) akimgawia miche Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Haji Mnasi (kulia)
 Sehemu ya miche ya miti waliyokabidhiwa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ileje
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiwa na sehemu ya miche waliyokabidhiwa na mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh Joseph Mkude.